Gwiji wa soka nchini Ufaransa Zinedine Zidane ameangukiwa na adhabu ya kufungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kuchukua jukumu la kukinoa kikosi cha wachezaji wa akiba wa klabu ya Real Madrid bila ya kuwa na vigezo vya kitaalum vinavyotakikana huko nchini Hispania.
Chama cha soka nchini humo kilibaini mapungufu hayo baada ya kufanya uchunguzi na kuona wazi Zidane akifanya kazi ya kukinoa kikosi cha wachezaji wa akiba cha Real Madrid Castilla sanjari na msaidizi wake Santiago Sanchez ambaye nae amekumbwa na adhabu ya kufungiwa.
Hata hivyo maamuzi hayo ya chama cha soka nchini Hispania yamepigwa na viongozi wa klabu ya Real Madrid na wameahidi kukata rufaa huku wakiamini adhabu hiyo itaondolewa dhidi ya wawili hao.
Uongozi wa Real Madrid umedai kwamba Zidane ana vigezo vyote vya kufanya kazi hiyo kwani alifaulu na kupitishwa na shiriksiho la soka nchini kwoa Ufaransa (FFF) na ndio maana walimkabidhi jukumu la kukinoa kikosi cha wachezaji wa akiba.
Zidane aliteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha wachezaji wa akiba mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuwa msaidizi wa meneja wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti msimu uliopita ambao ulimalizika kwa klabu hiyo ya mjini Madrid kutwaa ubingwa wa barani Ulaya.
Zinedine Zidane aliwahi kuwika akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa na kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1998, na aliitumikia klabu ya Real Madrid kama mchezaji, kwa muda wa miaka mitano baada ya kusajiliwa kwa ada ya uhamisho iliyoweka rekodi ya dunia mwaka 2001(Paund Milion 45.8) akitokea nchini Italia kwenye klabu ya Juventus
0 comments:
Post a Comment